Kama tatizo litakuwa langu, basi kwa moyo mweupe kabisa naomba nisaidiwe kueleweshwa, lakini kiukweli kuna baadhi ya maadhimisho tunayoyasherekea binafsi sioni mantiki yake kabisa, kwasababu baada ya kuadhimisha, haturudi kuyashughulikia, au kama tunarudi kuyashughulikia si katika kiwango chenye tija.
Ndio maana najiuliza kuna maana gani sasa ya kusherekea na kukumbushana, kama si ufujaji tu wa pesa za wananchi na wahisani katika kufanya sherehe hizo, jambo ambalo kama pesa hizo zingetumika katika kushughulikia matatizo hayo yanayoendana na siku hiyo tunayoisherekea, inawezekana kabisa zikawa zimeleta mabadiliko makubwa katika kukomesha matatizo hayo.
Kwa mfano; siku si nyingi zilizopita tuliadhimisha siku ya malaria duniani, ambapo serikali, taasisi na asasi zingine zisizo za kiserikali walifanya maadhimisho mbalimbali katika mikoa mbalimbali nchini.
Labda kwa mfano tu nizungumzie taasisi moja isiyo ya kiserikalli inayofadhiriwa na chuo kikuu kimoja cha Marekani, ambao wao walifanyia maadhimishio yao pale katika viwanja vya mnazi mmoja. Ni kweli kwamba walikutana, wakasomeana risala kukumbushana kuhusu tatizo, mziki ukapigwa na burudani zingine mbalimbali kama vile mchezo wa mpira wa miguu zikaambatana na maadhimisho hayo.
Lakini hebu tujiulize maswali; Hivi tunahitaji kutumia fedha hizo za wahisani kwa ajili ya kukutana mnazi mmoja kukumbusha kuhusu Malaria? Ni nani hapa nchini ambaye hajui, au amesahau kwamba malaria ipo na kila baada ya sekunde tano inaua mtanzania mmoja, tena mama mjamzito na motto wa chini ya miaka mitano ndio wahanga wakubwa wa ugonjwa huu? Ni nani ambaye amewahi kwenda hospitali kupimwa malaria na hajawahi kuambia hata siku moja kwamba anaumwa malaria? Ni nani ambaye hana ndugu yake hata mmoja ambaye amekufa kwa ajili ya malaria? Sasa kwanini kila mwaka tuwe tunakutana mnazi mmoja KUKUMBUSHANA kwamba malaria tunayo na inaua? Au huo mpira wa miguu tunaoucheza hapo mnazi mmoja, unauhusiano gani na kutokomeza malaria hii inayoua maelfu ya watanzania wenzetu kila siku?
I wish kama wangekuwa wanatutangazia bajeti za sherehe hizo, lakini pia nadhani ni bora tu hawatutangazii pesa zilizotumika kufanyia sherehe hizo, maana kwetu sisi wenye ugonjwa wa moyo inawezekana kabisa tungepata mshtuko halafu tukatangulia mbele ya haki kabla ya siku zetu.
Lakini vipi kama tungeweza kuzitumia pesa hizo kuongeza madawa za malaria hospitalini na kwamba kila mwananchi aweze kupata dawa hizo bure? Au kwanini tusingezichangachanga pesa hizo ambazo serikali na taasisi zote nchi huzitumia ‘kukumbushiana’ na tukanunua na kunyunyizia dawa kwenye mazingira yetu kutokomeza kabisa hawa mbu wanaoeneza malaria??
Kinachokera zaidi ni kwamba tunakutana mnazi mmoja kukumbushana, halafu tunasahau kwamba ni mwanakijiji wa LUCHELELE huku ndie anaepoteza maisha kila kunapoitwa leo kwasababu ya malaria kwa kukosa dawa au kukosa sh. 500 kununulia chandalua cha haki punguzo na kushindwa kufika hospitalini kutokana na umbali wa hospitali ilipo.
Kama kweli tunataka kukumbushana, kwanini tusiwafate wanakijiji hawa waliowahanga wakubwa wa vitu hivi tunavyokumbushana, ili tukawakumbushe vizuri? Kwanini tufanyie Mnazi mmoja na kila mwaka, katikati ya watu wanaojua A-Z juu ya malaria, na wamezungukwa na zahanati na hospitali kibao wanazoweza kwenda na kupatiwa matibabu ya malaria na wenye uwezo wa kununua hizo dawa za malaria na vyandarua pia?
Wakati leo hii tumebaki kuhadithiana na kuwatamani nchi zingine za magharibi kwa kukomesha malaria, nasikitika kwamba tunasahau kwamba wao hawakuiondoa malaria kwa kukutana tu na kukumbushana! Ilifika mahali wakachoka kukumbushana, wakaamua kuingia vitani kwa dhati kupambana na malaria. Wakaamua ‘kujipigapiga’ vijesenti walivyokuwanavyo, wakanyunyizia dawa kuzunguka mazingira yao, wakateketeza mazalia yote ya mbu wanaoeneza malaria, na leo hii Malaria ni historia kwao!
Sasa hebu niwaulize watanzania wenzangu, kujikumbusha kwetu huku kusikoisha, ni kwamba bado hatujaichoka hii malaria? Hivi kweli tumeamua kuitokomeza? Au ndio niamini kwamba wapo wale wenzetu wanaomba malaria hii iendelee kuwatafuna watu, isiishe, kwa sababu wao malaria hii inawapatia wao kula kwa kufanya kazi kwenye NGO’s za kukutanisha watu manazi mmoja kukumbushana juu ya malaria?
Kinachonishangaza zaidi ni kwamba ndugu zetu kabisa wa Zanzibar malaria wameanza kuiona kama historia. Ukifungua mitandao mingi ihusuyo malaria, utaikuta Zanzibar miongoni mwa nchi chache sana duniani zinazopigiwa mfano kwa kuitokomeza malaria. Sasa kitu gani kinachotushinda sisi kuiga mfano wao?
Kiukweli sikupanga kabisa kuzungumzia maadhimisho ya Malaria, lakini wakati nilipokuwa naendelea kuandika, nikakumbushwa vitu hivi ambavyo huwa vinanikera kila ninapovisikia maskioni mwangu.
Kikubwa kabisa kilichonisukuma kuandika, ni kesho tunapotarajia kusherehekea siku ya mtoto wa Africa. Nikakumbuka mambo yale yale ya kukutana mnazi mmoja na kukumbushana kwamba watoto wetu wanaishi katika mazingira magumu, wanazurura mitaani wakiombaomba msaada, hawaendi shule, lakini kwani ni nani asiyeyajua haya? Na kwasababu sasa tumeshakumbushana vya kutosha, ni lini tutaingia kwa dhati kuyashughulikia matatizo yao kama jamii kwa ujumla, badala ya kuwa kila mwaka tunakutana mnazi mmoja kukumbushana?
Mwanza bila shaka ni moja kati ya miji mikubwa nchini mwetu yenye idadi kubwa sana ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Ukitembea karibu kila mtaa mjini, utakutana na angalau watoto wawili ambao wanaishi katika mazingira magumu.
Siku moja niliwahi kuwauliza watu wanaofanya biashara maeneo ya mjini, ambao pia waliwahi kuwauliza watoto wenyewe sababu za wao kuondoka nyumbani kwao na kuja mtaani. Japo si mara zote watoto hawa ni wa kweli, lakini mara nyingi sababu ambazo wamekuwa wakizitoa ni sababu ambazo ziko ndani kabisa ya uwezo wa jamii yetu kuzipatia ufumbuzi.
Wengi wao wamekuwa wakilalamikia wazazi wao wa kambo (wazazi wakufikia), hasa mama, ambao wamekuwa wakiwatesa bila ya baba yao kujali. Lakini pia wengine wamekuwa wakisema wazazi wao wote wawili kufariki kwa ugonjwa wa UKIMWI, na hivyo wameachwa bila mtu wa kuwatunza na sababu nyingine kama hizo.
Lakini watu wazima wengi amabo kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakifuatilia tatizo hili, wamekuwa wakitaja sababu kama kuwepo kwa shughuli za uvuvi (hasa hapa Mwanza) ambazo zinawashawishi watoto kukimbia kwao, wakitaka kuja kufanya shughuli hizo kujipatia pesa na matokeo yake wanashindwa kuzifanya, lakini pia watoto wengi wanakimbia nyumbani kwao kwasababu hawapendi kwenda shule na sababu nyingine nyingi.
Binafsi nikiziangalia sababu hizi, naona zipi ndani kabisa ya uwezo wa jamii. Ndio maana naendelea kujiuliza swali, KWANINI JAMII TUSIAMUE KUKOMESHA SABABU HIZI WATOTO WETU WARUDI KUISHI NYUMBANI, WALELEWE KATIKA MAZINGIRA MAZURI? Nani bado anataka kuendelea kukumbushwa juu ya mazingira magumu wanayoishi watoto?
Wakati umefika sasa jamii tuliangalie upya swala hili la maadhimisho, na kukumbushana, na tuone haja sasa ya kuendelea kukumbashana huku tukichukua hatua za kuyatatua matatizo yetu, badala ya kuendelea kukumbushana huku tatizo likiwa pale pale au linazidi kuongezeka.
Tanzania yetu itajengwa na sisi wenyewe watanzania. Hakuna muhisani atakayekuja kutujengea kama sisi wenyewe hatuoni bado uhitaji wa kuijenga!
TANZANIA BILA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU, INAWEZEKANA!
Monday, June 14, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment